19
Jun 2026

HESLB YAFUNGUA DIRISHA LA MAOMBI YA MIKOPO 2026/2027

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dr. Bill Kiwia leo Juni 19, 2026 amefungua rasmi dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027, huku mchakato wa uombaji mikopo ukitarajiwa kuhitimishwa Agosti 31, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam Dr. Kiwia amesema, kufunguliwa kwa dirisha hilo kunakwenda sambamba na uzinduzi wa Miongozo minne (4) ya utoaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027.

“Miongozo hii imeandaliwa ili kuwasaidia waombaji kuelewa sifa, vigezo na taratibu za kupata mikopo na ruzuku. Tunasisitiza wanafunzi wasome na kuzingatia maelekezo yote yaliyomo kabla ya kuanza kujaza fomu za maombi kupitia mfumo wa OLAMS,” amesema Dr. Bill.

Miongozo iliyozinduliwa ni pamoja na ule wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Shahada za Awali, Stashahada, Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) pamoja na Mwongozo wa Ruzuku za Samia Scholarship.

Dr. Bill ametanabaisha zaidi kwamba, waombaji wanapaswa kuhakikisha wanatumia namba sahihi ya mtihani wa Kidato cha Nne wakati wa kuomba mkopo na kwamba namba hiyo ndiyo itakayotumika pia wakati wa kuomba udahili katika taasisi za elimu ya juu.

“Tunawakumbusha waombaji kuhakiki vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi (kwa wale waliofiwa na wazazi) kupitia RITA au ZCSRA na kupata namba za uhakiki kabla ya kuwasilisha maombi yao HESLB,” alisema.

Aidha, amewasihi waombaji wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wanapaswa kuwasilisha Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) pindi wanapojaza fomu za maombi ya mkopo, na kuwatoa hofu wale ambao bado hawajafikisha umri huo kuwa wataruhusiwa kuendelea na maombi hata kama hawana namba hiyo.

Katika hatua nyingine, HESLB itaendelea kutumia mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) katika utambuzi wa waombaji, wazazi na wadhamini wao ili kuongeza ufanisi na usahihi wa taarifa zinazowasilishwa.

Kuhusu Ruzuku za Samia Scholarship, Dr. Bill amesema wanafunzi 1,000 watakaofanya vizuri zaidi katika tahsusi za Sayansi kwenye mitihani ya Kidato cha Sita ya mwaka 2026 watanufaika na ufadhili huo wa Serikali.

“Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, Serikali itaendelea kuwatambua na kuwasaidia wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi kupitia mpango wa Samia Scholarship,” alisema.

HESLB pia imewahakikishia wanafunzi huduma za msaada kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja kitakachokuwa kinapatikana kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kila siku katika kipindi chote cha maombi.

Akihitimisha, Mkurugenzi Mtendaji huyo aliwataka wanafunzi kutotegemea dakika za mwisho kuwasilisha maombi yao.

“Muda wa kuomba mkopo ni wa kutosha. Tunawasihi waombaji kutumia vizuri kipindi hiki kwa kujaza taarifa sahihi na kupakia nyaraka zote zinazohitajika ili kukamilisha maombi yao ndani ya muda uliopangwa,” alisema.

Dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027 litakuwa wazi kwa siku sabini na tatu (73) kuanzia leo na litafungwa rasmi Agosti 31, 2026.

Published: June 19, 2026 at 11:20 AM