19
Jun 2026

Waajiri 11 Wapewa Tuzo na HESLB

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia leo ametoa tuzo kwa Waajiri 11 kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa kuonesha uwajibikaji mkubwa katika kuzingatia sheria ya HESLB, hususan katika kuwasilisha taarifa za waajiriwa wapya na makato ya mikopo kwa wakati.

Tuzo hizo zimetolewa, katika hafla fupi iliyofanyika leo (Ijumaa, Juni 12, 2026) katika ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki zilizopo jijini Dar es salaam.

Katika hotuba yake, Dkt. Kiwia amebainisha kuwa waajiri hao 11 waliotambuliwa na kupewa tuzo, wameonesha kwa vitendo, kwa kuhakikisha taarifa za waajiriwa wapya zinawasilishwa kwa wakati na makato ya mikopo yanawasilishwa kama sheria ya Bodi ya Mikopo inavyooelekeza.

“Leo ni siku ya kipekee kwa HESLB. Tumekusanyika si tu kwa ajili ya kutoa tuzo, bali pia kutambua mchango mkubwa wa waajiri katika kufanikisha dhamira ya Taifa ya kuwekeza katika mikopo ya elimu ya juu,” amesema Dkt. Kiwia na kuongeza kuwa, “Kupitia uwajibikaji wenu, mnachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mfuko wa mikopo na kuongeza uwezo wa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wanaohitaji msaada wa kifedha ili kupata elimu ya juu,”.

Taasisi za waajiri waliopata tuzo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), NMB Bank Plc, BRAC Tanzania Finance Ltd, CRDB Bank, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), National Bank of Commerce Limited, Tanzania Empowerment Forum Ltd, Vodacom Tanzania, Shifaa Pan African Hospital, Ishik Medical and Education Foundation na Mohammed Enterprises Tanzania Ltd.

Kuhusu umuhimu wa kurejeshwa kwa mikopo ya elimu ya juu, Dkt Kiwia amesema kuwa fedha zinazorejeshwa na wanufaika wa mikopo hutumika tena kuwasaidia wanafunzi wengine wapya wenye sifa, hivyo kila mwajiri anayewasilisha taarifa za waajiriwa wapya na kuwasilisha makato yao ya mikopo kwa wakati ni mchangiaji wa moja kwa moja katika kutimiza ndoto za vijana.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB, Bi. Shazmin Mehboob, amewashukuru waajiri hao 11 kwa kuzingatia sheria ya HESLB na kuwasilisha makato ya waajiriwa wao kwa wakati. Pia ametoa wito kwa waajiri wengine kuiga mfano mzuri wa waajiri hao.

Akiongea kwa niaba ya waajiri waliopewa tuzo, Naibu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Tija Ukondwa, ameishukuru HESLB kwa kutambua mchango wa mamlaka hiyo. Amebainisha kuwa TRA inaamini kwa dhati katika uzingatiaji wa sheria, jambo linalofanya masuala ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu kuchukuliwa kwa umuhimu mkubwa.

“Mtu akifanya vizuri na kutambuliwa, inampa motisha ya kufanya vizuri zaidi. Hivyo basi, TRA tunaahidi kuendelea kuzingatia sheria za Bodi ya Mikopo na kuwa mabalozi bora kwa waajiri wengine,” amesisitiza Bi. Tija.

Uzingatiaji wa Sheria ya HESLB unaendelea kuwa nguzo muhimu ya uendelevu wa mfuko wa mikopo ya elimu ya juu. Kila marejesho yanayofanyika kwa wakati huchangia moja kwa moja kupanua wigo wa kuwafikia Watanzania wengine wenye ndoto ya kusoma elimu ya juu.

Menejimenti ya HESLB imejiwekea utaratibu wa kuwatambua waajiri wanaozingatia sheria ya HESLB kwa kuhakikisha wanawasilisha majina na makato ya mikopo ya wanufaika waliowaajiri kwa wakati jambo ambalo limekuwa chachu ya kupanda kwa makusanyo ya mikopo mwaka hadi mwaka.

Published: June 19, 2026 at 11:17 AM