Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, zinajipanga kuanza awamu ya tatu ya mafunzo ya uombaji wa mikopo kwa usahihi kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita, kidato cha nne au shashahada kwa siku tatu mfululizo katika Viwanja vya Madungu, Pemba kuanzia Juni 1 hadi 3, 2026.
Pemba ni kituo kinachofuata baada ya kuhitimisha wiki mbili za mafunzo hayo yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia tarehe 20 hadi 29 Mei, 2026.
Awamu ya kwanza ilianza tarehe 20 hadi 22 Mei, 2026 katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Mtwara; awamu ya pili ikafuatia tarehe 25 hadi 29 Mei, 2026 katika mikoa ya Dar es salaam, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya na Morogoro.
Awali, akizungumza na wanahabari mnamo Mei 18, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu ya kina kwa wanafunzi, wazazi na walezi kuhusu taratibu za kujaza fomu za maombi ya mkopo na kufafanua kuhusu nyaraka muhimu zinazohitajika ili kukamilisha maombi ya mkopo kwa usahihi.
Wadau wengine wa kimkakati wanaoshirikiana na HESLB katika utoaji huo wa elimu ni pamoja na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia huduma yake ya Anwani za Makazi (NaPA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili Ufilishi na Udhamini (RITA), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Shirika la Posta na Kampuni ya Simu Yas Tanzania.
Wakati wa utoaji wa elimu, miongoni mwa huduma zinazotolewa ni pamoja cheti cha kuzaliwa, Namba ya Utambulisho wa Taifa, Elimu ya Mlipa Kodi na TIN namba, anwani ya makazi, huduma za kibenki na huduma ya Internet.
Wanafunzi, wazazi na walezi wanaolengwa na wakazi wa Pemba, wanakaribishwa na kuhimizwa kushiriki ili kupata elimu sahihi kuhusu uombaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2026/2027.