25
May 2026

HESLB na BOT Kuzindua Programu ya Elimu ya Fedha kwa Wanafunzi

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), zimezindua rasmi utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha utoaji wa elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini baada ya taasisi hizo mbili za umma kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano (MoU). Uzinduzi huo umefanyika Jumatatu ya Mei 18, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya BOT jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba ameipongeza HESLB kwa kuendelea kubuni na kuimarisha programu zinazolenga kuwawezesha wanafunzi kupata stadi za kifedha zitakazowasaidia kusimamia fedha zao kwa ufanisi wakiwa vyuoni na hata baada ya kuhitimu masomo yao.

“Ninaipongeza HESLB kwa kutambua umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi na kwa kushirikiana na BoT katika utekelezaji wa mpango huu muhimu. Vilevile, ninathamini juhudi zilizofanywa na timu za wataalam kutoka taasisi zote mbili katika kuandaa Hati hii ya Makubaliano (MoU)”, amesisitiza Gavana Tutuba.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema kuwa, wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu watanufaika na programu maalum ya elimu ya fedha kupitia mfumo wa akaunti binafsi za wanafunzi unaojulikana kama Student’s Individual Permanent Account (SIPA).

Programu hiyo itatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha, uandaaji wa bajeti, uwekaji wa akiba, matumizi yenye tija ya mikopo, huduma za fedha kidijitali pamoja na ulinzi wa mtumiaji wa huduma za kifedha.

“Kupitia elimu hii ya fedha, ni matumaini yetu makubwa kuwa wanafunzi watajenga nidhamu ya matumizi ya fedha, kujiwekea mipango ya kifedha, kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, pamoja na kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo kwa wakati. Hii itasaidia kuongeza uendelevu na ustahimilivu wa mfuko wa mikopo ya wanafunzi na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kunufaika katika miaka ijayo”, amesema Dkt. Kiwia.

Uzinduzi wa utekelezaji wa makubaliano hayo unaenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha huduma jumuishi za kifedha na kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Published: May 25, 2026 at 4:46 PM