Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia amesema upo umuhimu wa kuweka jitihada za pamoja za kikanda katika utoaji na urejeshaji mikopo ili nchi zote za Afrika zinufaike katika ngazi ya elimu ya juu.
Dkt. Kiwia ameyasema hayo leo (Jumatano, Mei 13, 2026) alipokutana na ujumbe wa maafisa watano kutoka Sekretarieti ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini Uganda wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Bw. Birungi Christopher.
“Tunahudumia kundi la wateja wa aina moja na hivyo tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja kama kanda”, amesema Dkt. Kiwia.
Dkt. Kiwia ameongeza kuwa suala la urejeshaji mikopo halihusishi tu Sheria bali pia uhusiano mzuri na waajiri na wanufaika ambao ni muhimu kuwaelimisha ili watambue kuwa wana wajibu wa kurejesha mikopo ili inufaishe vijana wengine wa kitanzania wenye uhitaji.
Ujumbe huo wa Uganda upo nchini kwa ziara ya mafunzo hususan katika eneo la Urejeshaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kujifunza mbinu na mikakati ya kukusanya marejesho kwa ufanisi.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Bw. Birungi amesema kuwa licha ya urejeshaji mikopo, wamejiifunza
masuala kadhaa ambayo wangependa yafanyike pia nchini Uganda ili kuboresha urejeshaji mikopo nchini humo. Baadhi ya masuala hayo ni kuhuisha sheria, kuzingatia matumizi ya mifumo ya TEHAMA na kushirikiana na wadau wote katika mnyororo wa usimamizi wa mikopo ya wanafunzi.
Sekretarieti ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini Uganda ni Idara ndani ya Wizara ya Elimu na Michezo.