22
Apr 2026

HESLB na TPC zasaini Ushirikiano wa kutoa Huduma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Shirika la Posta Tanzania (TPC), leo (Jumatano, Aprili 22, 2026) zimesaini makubaliano ya kutoa huduma ya maombi ya mikopo ya wanafunzi nchi nzima njia ya mtandao.

Hafla ya kusaini makubaliano baina ya Taasisi hizo mbili za umma, imefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Posta jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na menejimenti za HESLB na TPC, pamoja na wanahabari.

Akizungumza katika hafla hiyo, Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo amesema kuwa Posta ina mtandao mkubwa nchi nzima na ipo tayari kuwahudumia kwa weledi wanafunzi wanaoomba mikopo.

“Tumefanya mabadiliko makubwa ili kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za matibabu na elimu … tunawashukuru wadau wanaotuamini na wanaotumia mtandao wetu kufikisha huduma ndani na nje ya nchi”, amesema Mbodo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema HESLB ilikuwa inatafuta suluhisho la kuwezesha waombaji mikopo nchi nzima na ametoa pongezi kwa TPC kwa kuharakisha mchakato wa makubaliano hayo.

“Tulikuwa tunatafuta suluhisho la kuwasaidia waombaji mikopo kutoka nchi nzima … tunafurahi kwamba Posta ina ofisi zaidi ya 350 na hivyo tunaamini waombaji wa mikopo watapata usaidizi stahiki kutoka kwa watoa huduma wa TPC”, amesema Dkt. Kiwia.

Ushirikiano kati ya TPC na HESLB umekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja kwa lengo la kurahisisha mchakato wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Awali, kabla ya maombi ya mikopo kufanyika kwa njia ya mtandao, wanafunzi walikuwa wanatuma nyaraka zao kupitia huduma ya EMS ya Posta, hatua iliyosaidia kuongeza usalama, kasi na uhakika wa uwasilishaji wa nyaraka.

Huduma za Posta zinahakikisha usalama wa taarifa za waombaji, utoaji wa huduma sahihi, pamoja na uwajibikaji na ufuatiliaji na kuwapa wanafunzi uhakika wa huduma bora.

Published: April 22, 2026 at 4:59 PM