Atoa Wito Urejeshaji Mikopo Kidogo Kidogo
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amezindua rasmi kampeni ya “Kiduchu” na kusisitiza umuhimu wa urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu unaozingatia uwezo wa kila mnufaika hususan katika sekta isiyo rasmi ili kuhakikisha uendelevu wa mfuko kwa manufaa ya vizazi vijavyo. Uzinduzi huo umefanyika leo, (Aprili 17, 2026), katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Kanda ya Mashariki, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Wanu amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano (kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026), Serikali imefanikiwa kutoa TZS 3.6 trilioni kwa wanafunzi wa vyuo ngazi ya elimu ya kati na ya juu, hatua iliyowezesha vijana wengi kupata elimu bila vikwazo vya kifedha. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanategemea kwa kiasi kikubwa urejeshaji wa mikopo hiyo.
Kwa upande wa makusanyo, amebainisha kuwa HESLB imeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mikopo kupitia juhudi mbalimbali za uhamasishaji, hatua inayolenga kuhakikisha kuwepo kwa mfuko endelevu wa kugharimia elimu ya kati na ya juu nchini.
Mhe. Naibu Waziri ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wanufaika, hususan wenye kipato cha chini, ambao hawajaanza au wamesitisha urejeshaji wa mikopo kutokana na hali zao za kiuchumi.
Kutokana na hali hiyo, Mhe. Wanu amezindua rasmi kampeni ya “Kiduchu” yenye kaulimbiu “Fresh, Tunasonga!”, inayolenga kuwahamasisha wanufaika kuanza kurejesha mikopo yao kwa kiasi kidogo walichonacho, kwa kuanzia TZS 5,000. Kampeni ya “Kiduchu”, imelenga kuwafikia wanufaika 135,186 wanaodaiwa jumla ya TZS 920 bilioni.
“Kiduchu ni kidogo ya kidogo … na upekee wake ni kuwafikia wanufaika wenye kipato cha chini ili waweze kurejesha mikopo yao kulingana na uwezo wao’’, amesema Mhe. Wanu na kuongeza, “Msisubiri hadi muwe na fedha nyingi … anzeni na kiduchu mlichonacho leo. Kila mchango, hata uwe mdogo kiasi gani, una mchango mkubwa katika kujenga taifa letu.”
Aidha, Mhe. Wanu amewahimiza waajiri, taasisi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na HESLB ili kuhakikisha wanufaika wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sharia, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA na kuongeza elimu kwa umma ili kuunga mkono juhudi hizo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB, Prof. Hamisi Dihenga, amesema kampeni hiyo inaakisi kaulimbiu ya “Kazi na Utu” kwa kuzingatia hali halisi ya kipato cha wanufaika.
“Kazi na Utu … imetufikisha hapa ili tuwafikirie wanufaika wenye kipato cha chini. Watu hatulingani”, amesema Prof. Dihenga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alieleza kuwa madeni yaliyoiva yanafikia TZS 2.78 trilioni kutoka kwa wanufaika 539,103, ambapo hadi sasa TZS 1.84 trilioni zimekusanywa kutoka kwa wanufaika 403,917 waliokwisha. Hata hivyo, bado kuna wanufaika 135,186 wanaodaiwa TZS 920 bilioni ambao hawajafikiwa.
Aidha, amebainisha kuwa katika robo ya tatu iliyoishia Machi 31, 2026, HESLB imekusanya TZS 175.9 bilioni, sawa na 106.% ya lengo la kukusanya TZS 165 bilioni, huku lengo la mwaka mzima likiwa TZS 220.3 bilioni.
Kwa upande wake mmoja wa wadau wa kimkakati, Mkurugenzi Mtendaji wa CreditInfo Tanzania, Bw. Edwin Urasa, amesema kampeni hiyo imekuja wakati muafaka kwani wadaiwa wengi wanatoka katika sekta isiyo rasmi, hivyo utaratibu wa kulipa kidogo kidogo utawawezesha kurejesha mikopo kwa urahisi zaidi.
Wengine walioshiriki katika uzinduzi huo walikuwa ni wadau kutoka taasisi za fedha na wanufaika walioko katika sekta isiyo rasmi akiwemo Bw. Paul Mlewa, mhitimu wa Shahada ya Ualimu katika masomo ya Uchumi na Hisabati mwaka 2016 katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), kampasi ya Dar es salaam. Paul ni mchekeshaji wa Kundi la WatuBaki anayejulikana kwa jina la “Teacher Paul” ambaye amekiri kuelewa kampeni hiyo na kwamba yuko tayari kuanza kurejesha
Akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo wa HESLB, Bw. George Mziray, amesema kabla ya “Kiduchu”, kulikuwa na kampeni ya “Sifurisha” iliyolenga kuhamasisha wanufaika kulipa mikopo yao kwa mkupuo, ikifuatiwa na kampeni ya “Fichua” iliyolenga kubaini wadaiwa ambao hawajaanza kurejesha mikopo na kuwahamasisha kujitokeza. “Kiduchu” inalenga kuziba pengo kwa kuwafikia wanufaika wenye kipato cha chini na kuwahamasisha kurejesha mikopo kidogo kidogo kulingana na uwezo wao.
Urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu unachangia kwa kiasi kikubwa kuendeleza mfuko wa elimu nchini, kwa kuwa fedha zinazorejeshwa hutumika kuwawezesha wanafunzi wengine wahitaji na hivyo kujenga mnyororo endelevu wa uwezeshaji na maendeleo ya taifa.