9
Apr 2026

Wanawake watumishi HESLB wakumbuka Watoto Kurasini

Wanawake watumishi wa HESLB wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake RAAWU - HESLB, Bi. Gertrude Alphonce (leo, Alhamisi Aprili 9, 2026), wametembelea katika kituo cha Makao ya Watoto kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam na kutoa misaada ya mahitaji mbalimbali yenye thamani ya TZS 5,000,000/-.

Akieleza nia ya kufika katika kituo hicho, Bi. Gertrude amesema kuwa HESLB imeguswa na hali ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu, jambo lililowasukuma kufanya matendo ya huruma kwa kutoa msaada katika kituo hicho.

Bi. Gertrude amesisitiza kuwa lengo si tu kusaidia mahitaji ya msingi bali pia kuwafanya watoto hao wajione wanatambuliwa, kuthaminiwa na kuwa na nafasi muhimu katika jamii inayowazunguka.

Akizungumza wakati wa mapokezi, Afisa Ustawi wa kituo hicho, Bw. Andrew Michael Haule, ameeleza kuwa kituo hicho ni cha pekee cha Serikali kilichopo katika Mkoa wa Dar es Salaam na kufafanua kuwa Watoto hao wanaishi kituoni hapo lakini hupata huduma za kijamii kama elimu na ibada nje ya kituo, jambo linalowajenga kuwa sehemu ya jamii.

Bw. Haule amesema, kwa sasa kituo hicho kina watumishi 19, ambapo wanawake ni 14 na wanaume 5 na pia kina jumla ya watoto 100, ambapo 60 ni wavulana na 40 ni wasichana, mtoto mwenye umri mdogo zaidi ana miaka mitano na tayari anasoma darasa la kwanza.

"Sisi wote ni walezi tumefurahia ujio wenu na tunashukuru sana kwa msaada huu mkubwa mliotuletea."  Amesisitiza Bw. Haule.

Aidha, ameonesha kufurahishwa kwake kwamba baadhi ya watoto waliowahi kulelewa kituoni hapo tayari wamenufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na wanaendelea na masomo vyuo vikuu.

"Kuna watoto wetu watatu kwa sasa ambao wananufaika na mikopo na wapo vyuo vikuu, jambo linalotupa matumaini makubwa," amesisitiza Bw. Haule.

Kituo cha Makao ya Watoto Kurasini, kilianzishwa na wamisionari kutoka Ujerumani mwaka 1966 na mwaka 1968 kikaanza kusimamiwa na Serikali. Hivi sasa kiko chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Kituo hicho kinaendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali inayolenga kuwahudumia watoto kwa kuwapatia malezi bora, elimu na mazingira salama ya kukua kwa kushirikiana na maafisa ustawi wa halmashauri, polisi, pamoja na vituo vya mabasi ili kuhakikisha watoto wenye uhitaji wanatambuliwa na kufikishwa mahali salama.

HESLB, ambayo ni taasisi ya serikali inayotoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji katika taasisi za elimu ya juu, imeendelea kuwa na desturi ya kuwafikia watu katika ngazi ya chini kabisa ya jamii, wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum na wanaolelewa katika mazingira magumu, ili kuwasaidia kujenga mustakabali bora na wenye matumaini ya maisha ya baadaye.

Published: April 9, 2026 at 12:22 PM