Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), leo (Alhamisi, Machi 26, 2026), imefanya kikao na taasisi mbalimbali zinazofadhili wanafunzi kikilenga kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanafunzi.
Akifungua kikao hicho ambacho kimefanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, jijini Arusha, Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema kimeandaliwa mahsusi ili kujenga ushirikiano madhubuti kati ya HESLB na taasisi zinazofadhili wanafunzi ili kuboresha ufanisi wa utendaji na kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanapata fursa ya elimu ya juu.
Dkt. Kiwia amezipongeza taasisi hizo kwa kuona umuhimu wa kuwasomesha wanafunzi wanaotoka katika kaya zenye kipato cha chini au zenye changamoto mbalimbali, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika maendeleo ya taifa na ameongeza kuwa kikao hicho kitakuwa ni endelevu na kitafanyika kila mwaka ili kuimarisha mahusiano, kuboresha huduma kwa wanafunzi, na kuangalia namna bora ya kushirikiana na taasisi zinazofadhili wanafunzi katika ngazi ya sekondari ili kuendeleza ushirikiano huo hadi elimu ya juu.
“Tunaamini kuwa kwa kuimarisha ushirikiano huu, tutafanikiwa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji, kuunganisha nguvu zetu katika kuwahudumia, na kuweka misingi imara ya maendeleo ya elimu ya juu nchini,” amesema Dkt. Kiwia.
Aidha, Dkt. Kiwia ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa za kuwekeza katika elimu ya juu ambapo zaidi ya TZS 3.6 trilioni zimetolewa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa HESLB, zaidi ya Watanzania milioni moja (1) wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao za kielimu.
Akizungumzia matarajio ya HESLB baada ya kikao hicho, Dkt. Kiwia amesema matokeo ya kikao hicho yatawezesha kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa sahihi na kuweka kumbukumbu kidijitali kwa ufanisi zaidi, kushirikiana na wadau ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi, kupanua wigo wa ufadhili wa elimu ya juu, pamoja na kupokea maoni yatakayosaidia kuboresha mifumo ya ufadhili na utoaji wa huduma kwa wanafunzi.
Awali, mwenyeji wa kikao hicho kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof. Suzana Augustino ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, amesema wanafurahi kwa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu.
Prof. Suzana amewakaribisha washiriki wote na wadau mbalimbali kufika chuoni hapo kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu, akibainisha kuwa lengo la taasisi hiyo ni kuwa kituo kikubwa cha utafiti wa kisayansI na ubunifu. Aidha, ameishukuru HESLB kwa mchango wake katika elimu kwani yeye pia ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo.
Kwa ujumla, kikao hicho ambacho pia kimetumika kukabidhi vyeti vya usajili kwa taasisi 305 zinazotambuliwa na HESLB, kimeonesha umuhimu mkubwa wa ushirikiano kati ya HESLB na wadau wa ufadhili wa elimu, ambapo kwa pamoja wanaweza kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji na kuwawezesha kupata elimu ya juu, hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.