Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


6
June 2024

Msimu wa Uombaji Mikopo kwa mwaka 2024/2025 Wafunguliwa

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia leo (Alhamisi, June 06, 2024), amezungumza na vyombo vya Habari kuhusu kufunguliwa kwa msimu wa uombaji mikopo kwa mwaka 2024/2025 na kuweka wazi jinsi HESLB ilivyojipanga kutoa huduma kwa waombaji mikopo wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu katika ngazi tofauti tofauti.

Miongozo ya Utoaji Mkopo na Muda wa dirisha la maombi kuwa wazi

Dkt. Kiwia aliwakumbusha wanahabari kuhusu miongozo mitano ya utoaji mikopo iliyozinduliwa Mei 27, 2024 na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda (Mb), kuwa ni pamoja na;

        i. Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Shahada ya Awali (Bachelor) kwa 2024 -2025,

        ii. Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Stashahada (Diploma) kwa 2024 – 2025,

        iii. Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Stashahada ya Umahiri katika Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo  kwa 2024 – 2025 (Post Graduate Diploma in Legal Practice),

        iv. Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Shahada za Umahiri na Uzamivu, na

         v. Mwongozo wa Utoaji Ruzuku za Samia kwa mwaka 2024 - 2025

“Miongozo hiyo inapatikana kwenye tovuti yetu ya Bodi ya Mikopo ya www.heslb.go.tz  toka Juni 01, 2024 na nawasihi waombaji mikopo kusoma na kuielewa miongozo hiyo kabla ya kuanza kufanya maombi ya mkopo, pamoja na kuzingatia muda uliopangwa wa kujaza maombi ya mkopo wa siku tisini (90), kuanzia Juni 01 hadi Agosti 31, 2024”, amesisitiza Dkt. Kiwia.

Huduma kwa Wateja

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia ameelezea jinsi HESLB ilivyojipanga kutoa huduma kwa waombaji mikopo kwa kuwa na dawati maalum la kusaidia wateja wanaokwama wakati wa kujaza maombi yao au kuhitaji ufafanuzi zaidi kwa kupiga simu kwenye namba 0736 665 533 au kutuma ujumbe wa “WhatsApp’’ kwenda namba 0739 665 533.

Katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, serikali imetenga TZS 787 bilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa jumla ya wanafunzi 250,000. Idadi hii ya wanafunzi imeongezeka kutoka wanafunzi 224,056 mwaka 2023/2024. Hivyo, kwa mwaka ujao wa masomo kutakuwa na ongezeko la jumla ya wanafunzi 25,944.