Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


22
June 2023

TAARIFA:DIRISHA LA KUPOKEA MAOMBI YA MKOPO KWA MTANDAO HALIJAFUNGULIWA

Tunapenda kuwataarifu wanafunzi wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu unaotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kuwa dirisha la kupokea maombi kwa njia ya mtandao HALIJAFUNGULIWA.

Taarifa hii inalenga kutoa ufafanuzi kutokana na taarifa potofu zilizoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia jana, Juni 21, 2023 kuwa maombi ya mkopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na shahada, stashahada na astashahada yameanza kupokelewa na tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni Agosti 31, 2023.

Kwa sasa, kama tulivyoeleza katika Taarifa kwa Umma iliyotolewa Juni 2, 2023 ambayo pia inapatikana katika www.heslb.go.tz, HESLB inakamilisha ‘Mwongozo wa Utoaji Mkopo kwa Mwaka nwa Masomo 2023/2024’ ambao utapatikana katika tovuti ya HESLB kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Julai, 2023.

Mwongozo huo utaeleza kwa kina sifa za kupata mkopo, utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao, njia za kupokea mrejesho ikiwemo akaunti binafsi ya mwombaji mkopo inayojulikana kama ‘SIPA’ – Student’s Individual Permanent Account.

Aidha, wakati waombaji mkopo wakisubiri Mwongozo, kwa sasa, wanashauriwa kujiandaa kwa kuhakikisha yafuatayo:

1. Kuwa na akaunti ya benki yenye majina sawa na yaliyomo kwenye cheti chake cha kidato cha nne;

2. Kuwa na namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake ambayo ataitumia akiwa chuoni;

3. Kuhakiki cheti chake cha kuzaliwa kwa kufuata maelekezo ya RITA (Tanzania Bara) au ZCSRA (Zanzibar);

4. Kuandaa nakala ya kitambulisho cha mdhamini wake; kinaweza kuwa kimoja kati ya NIDA, Kadi ya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Pasi ya Kusafiria, au Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi;

5. Kuandaa picha ndogo za rangi (pass-port size) za mwombaji mkopo na mdhamini wake; na

6. Kuandaa namba yake ya NIDA. Kama mwombaji hana kwa sasa, HAITAMZUIA kufanya maombi ya mkopo.

Tunawashauri wanafunzi waombaji mkopo kuwa watulivu na kufuatilia taarifa rasmi kutoka HESLB zinazopatikana kupitia www.heslb.go.tz na katika mitandao ya kijamii ya Instagram, Twitter na Facebook kupitia ‘HESLB Tanzania’.

 

Imetolewa na:

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,

Jengo la PSSSF, Ghorofa ya Nne,

Barabara ya Makole,

S.L.P. 984,

DODOMA