Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


22
October 2021

WANAFUNZI 7,364 WAPANGIWA MIKOPO YA TZS 19.4 BILIONI KATIKA AWAMU YA PILI

Ijumaa, Oktoba 22, 2021

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza leo (Ijumaa, Oktoba 22, 2021) orodha ya awamu ya pili yenye wanafunzi 7,364 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 19.4 Bilioni kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa orodha hiyo iliyotolewa leo inafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza kufikia 45,095 waliopangiwa mikopo yenye kiasi cha thamani ya TZS 119.3 Bilioni.

Badru ameongeza kuwa HESLB tayari imeanza kupeleka fedha za wanafunzi hao waliopangiwa mikopo awamu ya pili katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru.

Tarehe ya kutolewa Orodha ya Awamu ya Tatu

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Tatu, Badru amesema orodha ya wanafunzi waliopangiwa mikopo itatolewa Jumatatu, Oktoba 25, 2021 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Orodha hii ya pili inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wamekamilisha taratibu za udahili wa chuo kimoja … tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya tatu katika siku tatu zijazo, yaani Jumatatu Oktoba 25, 2021,” amesema Badru.

TZS 570 Bilioni zimetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2021/2022

Kwa mujibu wa Badru, Serikali imetenga TZS 570 Bilioni kwa ajili ya mikopoya jumla ya wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka. 

Fedha zimeanza kutumwa vyuoni

Wakati huohuo, Badru amesema HESLB imeshapokea fedha kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na taratibu za malipo zimekamilika na fedha za wanafunzi zinatarajia kufika vyuoni kuanzia leo, Ijumaa Oktoba 22, 2021.

Wito

Aidha, Badru alisema HESLB inawasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Mwisho.

Imetolewa na:

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

DAR ES SALAAM

Ijumaa, Oktoba 22, 2021