Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


1
September 2021

HESLB YAONGEZA MUDA WA SIKU 15 UOMBAJI MIKOPO

Waliopo JKT kupewa fursa kuanzia Septemba 20 hadi 30

Dar es salaam, Septemba 1, 2021

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa uombaji mikopo kwa siku 15 zaidi kuanzia Septemba 1 hadi 15 mwaka huu ili kuwapa fursa kwa waombaji mikopo ambao wamejisajili katika mfumo kukamilisha maombi yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru ametangaza uamuzi huo leo (Jumatano, Septemba 1, 2021) jijini Dar es salaam na kufafanua kuwa uamuzi huo umetokana na maombi na ushauri walioupokea kutoka kwa wadau.

Idadi ya waombaji

“Tulianza kupokea maombi kwa njia ya mtandao Julai 9, mwaka huu na hadi jana ambayo ilikua siku ya mwisho ya kuomba tulikua na waombaji 91,445 waliowasilisha maombi, na kati ya hayo, maombi 12,252 yalikua hayajakamilika na wateja wetu wameomba muda wa kukamilisha,” amesema Badru.

Mkurugenzi Mtendaji alikua akiongea katika mkutano na wanahabari uliofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam ambao pia ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambao pia wanawahudumia waombaji mkopo.

Hatua inayofuata

Kwa mujibu wa Badru, hatua inayofuata ni uhakiki wa nyaraka na taarifa zilizowasilisha na waombaji 79,193 ambao maombi yao yamekamilika kama yanavyoonekana kwenye mfumo.

“Kuna makundi mawili, wale 12,252 ambao maombi hayana viambatisho na hivyo hayajakamilika … na kuna maombi 79,193 yenye nyaraka, sasa tunaanza kuhakiki usahihi wake na baadae tutaangalia kama wamepata udahili na wale wenye sifa ndiyo watapangiwa mkopo,” amesema Badru.

Fursa ya kuomba mkopo vijana waliopo JKT

Kuhusu wanafunzi wahitaji wanaoendelea na mafunzo katika Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Badru amesema vijana hao waliopo katika kambi 19 nchini watapata fursa ya kuomba mkopo kwa siku 10 kuanzia Septemba 20 hadi 30 mwaka huu.

“Tumekuwa tukiwasiliana na Makao Makuu ya JKT, na tumekwenda na kukutana na vijana hao katika kambi zote na tuliwaahidi kuwa watapata fursa … ambayo ni kuanzia Septemba 20 hadi 30 mwaka huu, hivyo wasiwe na wasiwasi,” amesema Badru.

RITA na TPC kuendelea kuwahudumia waombaji

Katika mkutano huo, Badru pia ameeleza kuwa HESLB imekubaliana na RITA na TPC kuendelea kuwahudumia waombaji mkopo katika kipindi chote kilichoongezwa.

“Wenzetu wa RITA wanaendelea kuhakiki vyeti vya vifo na kuzaliwa wanavyopokea na wamekuwa wakifanya hivyo hata kabla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi … na Posta (TPC) wameahidi kuendelea kupokea nyaraka kupitia huduma ya EMS katika muda ulioongezwa, tunawashukuru sana” amesema Badru.

Bajeti ya mikopo kwa 2021/2022

Katika mwaka wa masomo 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha TZS 570 Bilioni kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi 160,000 wa taasisi za elimu ya juu. Kati ya hao, wanafunzi 62,000 wanatarajiwa kuwa ni wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 98,000 wanaoendelea na masomo. Bajeti kwa mwaka 2020/2021 ilikua TZS 464 bilioni na zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 149,398.

Imetolewa na:

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,

Dar es salaam, Jumatano, Septemba 1, 2021