Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) leo Ijumaa Mei 16, 2025, wamefanya kikao na waandishi wa habari katika ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki zilizopo Dar es Salaam kwa lengo la kuutarifu umma kuhusu kuanza kushirikiana kuwapatia namba ya utambulisho (NIN) wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026.
Akiongea kwenye kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia, ameweka wazi kuwa namba ya utambulisho wa taifa itakuwa ni ya lazima katika kuomba mkopo kwa mwaka ujao wa masomo. “Tunatarajia kufungua dirisha la maombi ya mkopo mwezi Juni, 2025… kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 … namba ya utambulisho wa taifa itakuwa hitaji la lazima katika kujaza fomu za maombi ya mkopo, hivyo waombaji wote wanapaswa kuwa na namba hii wakati wa kujaza maombi yao ya mkopo”, amesema Dkt. Kiwia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Bw. James Kaji, amesema kuwa NIDA wapo tayari kuwahudumia wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na kuomba mikopo kutoka HESLB kwa kuwapatia namba za utambulisho kwa wakati na hivyo wanafunzi wanapaswa kufika kwenye ofisi za NIDA mapema ili kupatiwa namba za utambulisho. “NIDA ni maisha, kwa sasa … NIDA inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha mifumo yote ya serikali inasomana… tunawasisitiza waombaji wote wa mikopo ya elimu ya juu kuhakikisha wanafika mapema NIDA ili kupata namba ya utambulisho wa taifa”, ameeleza Bw. Kaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya namba ya utambulisho kwenye uombaji mkopo kuwa itasaidia kupata taarifa za uhakika za waombaji mikopo na katika urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi mara wanapohitimu elimu zao. “Tayari wataalaamu wetu wa mifumo kutoka HESLB na NIDA wamekalimisha kuunganisha mifumo, ili kuhakikisha waombaji wote wa mikopo wanajaza namba za utambulisho katika maombi yao ya mkopo, na kupata taarifa za uhakika za waombaji mikopo ambazo pia zitasaidia katika urejeshaji wa mikopo”, amesisitiza Dkt. Kiwia
Kuhusu kurahisisha huduma kwa waombaji wa namba za utambulisho wa taifa, Bw. Kaji amesema NIDA imeboresha huduma kwa njia ya mtandao na kusisitiza waombaji wa namba za utambulisho wa taifa (NIN) kuingia kwenye mtandao wa NIDA kwa kutumia kiunganishi https://eonline.nida.go.tz ili kuwasilisha maombi yao. “Waombaji wa namba za utambulisho wa taifa wanaweza kuomba kupitia mtandapo wa NIDA…njia hii ya mtandao inarahisisha sana na kupunguza foleni kwenye ofisi za NIDA kwa kuwa 75% ya usajili inafanywa na mwombaji mwenyewe kupitia njia ya mtandao na 25% itafanywa na ofisi ya NIDA”, amefafanua Bw. Kaji.
HESLB na NIDA wamejipanga kuanza kutoa elimu kuhusu umuhimu na namna kupata namba ya utambulisho wa taifa kwa kuanza na mkoa wa Dar es Salaam ili kurahisisha zoezi la kutoa namba kwa waombaji wa mikopo wanaotarajia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka 2025/2026.