Higher Education Students' Loans Board
Machi 18, 2024, Dar es salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) zimesaini hati ya makubaliano yenye lengo la kutafuta fursa za ajira kwa wanufaika na mikopo ya elimu ya juu ili kuwawezesha kurejesha.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika leo (Jumatatu, Machi 18, 2024) katika ofisi za HESLB zilizopo posta jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB Prof. Hamisi Dihenga, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA Juma Burhan Mohamed na watendaji wengine kutoka HESLB na ZEEA.
“Pamoja na fursa za ajira, tunaingia mashirikiano haya ili kuongeza kasi ya urejeshaji mikopo kutoka kwa wajasiriamali walionufaika na mikopo ya elimu ya juu na pia kuashiria nia njema na kuongeza ufanisi kupitia mashirikiano ya kimkakati kama tunavyoelekezwa na viongozi wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi,” amesema Dkt. Kiwia katika hafla hiyo.
Dkt. Kiwia amesema, kupitia makubaliano hayo, HESLB itaendelea kuwawezesha vijana kupata elimu kupitia mikopo na ZEEA itawaongezea ujuzi kupitia vituo atamizi (incubation centres) ili kuwaongezea ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa katika sekta binafsi hususan katika Utalii na Uchumi wa Buluu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed amesema taasisi yake inawajengea vijana uwezo kupitia vituo atamizi vilivyopo Zanzibar ambavyo vinalenga kuwaongezea ujuzi wahitimu wa vyuo vikuu.
“Tulikutana tarehe 28 Februari mwaka huu kwa mara ya kwanza, lakini kwa vile pande zote mbili tumeonesha utayari ndiyo maana leo tumeweza kufikia hatua hii ya kusaini makubaliano yatakayowezesha ufanisi zaidi kwa taasisi zetu”, amesema Mkurugenzi Mohamed.
ZEEA ni taasisi ya umma iliyoanzishwa mwaka 2022 ili kuwawezesha wananchi kiuchumi. Aidha, HESLB ilianzishwa mwaka 2004 ili kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.