Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


29
October 2021

HESLB YATANGAZA ORODHA YA NNE YENYE WABUFAIKA 5,003

Wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 11.6 bilioni

Wanufaika mwaka wa kwanza sasa wafikia 65,359

 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Ijumaa, Oktoba 29, 2021) imetangaza Orodha ya Nne yenye wanafunzi wapya 5,003 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 11.6 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amewaeleza wanahabari jijini Dar es salaam kuwa baada ya kutangazwa kwa orodha hiyo, jumla ya wanufaika wa mwaka wa kwanza sasa imefikia 65,359 ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 168.9 bilioni.

“Orodha hii ya nne ina wanufaika 5,003 ambao muda wowote kuanzia sasa wanaweza kuingia katika akaunti zao za SIPA walizoombea mkopo na kupata taarifa zaidi,” amesema Badru katika mkutano na wanahabari uliofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam.

Akifafanua zaidi kuhusu wanufaika hao 65,359, Badru amesema wanufaika 1,133 ni yatima waliofiwa wazazi wawili; 9,450 waliofiwa na mzazi mmoja; 198 ni wanafunzi wenye ulemavu; 2,919 walifadhiliwa na taasisi mbalimbali katika masomo yao ya sekondari; na 51,559 wanatoka katika kaya masikini.

“Kwa takwimu hizi, mtaona kuwa ile dhamira ya Serikali kuwawezesha vijana kutoka kaya masikini inathibitika,” amesema Badru na kuongeza kuwa asilimia 41 ya wanufaika 65,359 ni wanawake na asilimia 59 ni wanaume.

Mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo

Wakati huohuo, Badru amesema kuwa HESLB inakamilisha malipo ya wanafunzi 74,440 ambao ni wanufaika wanaoendelea na masomo baada ya kupokea matokeo yao ya mitihani yanayothibitisha kuwa wamefaulu kuendelea na masomo.

“Tuna wanufaika zaidi ya 98,000 wanaoendelea na masomo na hadi leo (Ijumaa, Oktoba 29, 2021) tumeshapokea matokeo ya mitihani ya wanafunzi 74,440 waliofaulu na tutaanza kutuma fedha kesho,” amesema Badru na kuvikumbusha vyuo kuwasilisha matokeo ya wanufaika waliobaki.

Dirisha la Rufaa

Kuhusu hatua inayofuata, Badru amesema dirisha la rufaa litafunguliwa Novemba 6, 2021 ili kuwapa fursa wanafunzi ambao hawajaridhika na viwango vya mikopo vya sasa kuwasilisha maombi ya kuongezewa.

Wanaoendelea na masomo na wameomba mkopo kwa 2021/2022

“Tumekua tukipokea maswali kuhusu wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wameomba mkopo mwaka huu … tunakamilisha orodha yao na tutaitoa siku chache zijazo baada ya kujiridhisha na uhitaji wao na kuthibitisha kuwa wamefaulu mitihani yao na matokeo yao yamewasilishwa kwetu,” amefafanua Badru.

Elimu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza

Katika hatua nyingine, Badru amesema maafisa wa HESLB wanaendelea na mikutano na wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopo vyuoni ili kuwaelimisha kuhusu taratibu za malipo na kufafanua masuala mbalimbali yanayojitokeza.