29
Jan 2026

HESLB Yazindua “BWANABOOM” Kuboresha huduma kwa wadau

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Januari 28, 2026) imezindua rasmi mfumo wezeshi wa huduma kwa wateja kwa kutumia akili unde unaojulikana kwa jina la BWANABOOM, unaolenga kuboresha na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wadau wa elimu nchini kwa saa 24 kila siku.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia (WyEST), Profesa Daniel Mushi, alikuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya HESLB jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Menejimenti ya WyEST ikiongozwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Maryam Ismail na Menejimenti ya HESLB. Wengine waliohudhuria walikuwa ni wawakilishi wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha St. John’s na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Mushi ameisifu HESLB kwa juhudi zake za kuendelea kubuni na kuendeleza mifumo ya kiteknolojia ambayo imekuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wa elimu nchini.

“Leo tunaongeza huduma ya Akili Unde ‘BWANABOOM’ kama njia nyingine muhimu ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wadau kuwasiliana moja kwa moja na HESLB kwa njia hii ya kidigitali. Hili ni jambo la kujivunia na linapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini’, amesema Prof. Mushi.

Ameipongeza HESLB kwa maono na ubunifu wake katika utoaji wa huduma kwa Watanzania, hususan wanafunzi wa elimu ya juu, akibainisha kuwa mfumo huo wa huduma kwa kutumia akili unde ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidigitali katika sekta ya elimu.

Aidha, Prof. Mushi amesisitiza kuwa kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, ni muhimu kwa HESLB kuendelea kuboresha huduma zake, kuimarisha ulinzi na usalama wa taarifa, pamoja na kuandaa mikakati itakayowezesha matumizi ya lugha ya ishara ili kuwahudumia ipasavyo wadau wenye mahitaji maalumu.

“Ni muhimu mkumbuke kuwa teknolojia inabadilika kwa kasi kubwa … ninatoa wito kwenu kuendelea kuboresha huduma zitolewazo kupitia BWANABOOM, kuhakikisha usalama wa taarifa binafsi unazingatiwa kikamilifu, kuendelea kupima kiwango cha kuridhika kwa wateja ili kuboresha zaidi huduma, na kuangalia uwezekano wa kuanzisha lugha ya ishara ya kidigitali, ili Watanzania wenye ulemavu wa kusikia, waweze kupata huduma kupitia ‘BWANABOOM’, amesisitiza Prof. Mushi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema ubunifu wa BWANABOOM ni sehemu ya safari ya kimkakati wa taasisi hiyo anayoiongoza katika kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa, kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa upatikanaji wa taarifa.

Naye Bi. Jaqueline Humbaro ambaye ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) na mwanafunzi wa Sheria, mwaka wa nne, amesifu ubunifu huo na kuahidi kuwashirikisha na kuwahimiza wanafunzi wenzake kuutumia ili kunufaika na huduma hiyo mpya na ya kisasa.

Mfumo wa BWANABOOM unatarajiwa kurahisisha utoaji wa huduma kwa wadau wa elimu, kupunguza gharama za usafiri na muda, huku taarifa muhimu zikisogezwa karibu zaidi na wananchi kupitia tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na akaunti za mikopo za wanafunzi maarufu ‘SIPA’. Mfumo huu unaonesha dhamira ya HESLB katika kutumia teknolojia ya akili unde kama nyenzo ya kiteknolojia ya kuboresha maendeleo ya elimu nchini.

Published: January 29, 2026 at 6:29 PM