Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, (Ijumaa, Machi 6, 2026) ameshiriki futari (Iftar) iliyoandaliwa na watumishi wanawake wa HESLB katika Hoteli ya King Jada, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Iftar hiyo, Dkt. Kiwia aliwapongeza wanawake wafanyakazi wa HESLB kwa kuandaa tukio hilo muhimu, akieleza kuwa ni fursa nzuri ya kukutana, kubadilishana mawazo na kuendelea kuimarisha umoja ndani ya taasisi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa wanawake katika maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujiamini na kutumia uwezo wao kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Kiwia pia alisisitiza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika kuifikia Dira ya Taifa 2050, akieleza kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Alibainisha kuwa kila mwanamke ana haki ya kupata fursa sawa katika elimu na ajira, na kwamba mafanikio ya jamii kwa ujumla yanategemea ushirikiano wa watu wote, wakiwemo wanawake.
“Idadi ya wanawake katika jamii ni kubwa, hivyo ushiriki wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo ni muhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya 2050. Wanapaswa kupewa fursa sawa katika elimu na ajira ili kuchochea maendeleo ya jamii,” amesisitiza Dkt. Kiwia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake kupitia Chama cha Wafanyakazi (RAAWU) tawi la HESLB, Bi. Gertrude Alphonce, alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwawezesha wanawake wa HESLB waliopo Dar es Salaam na ofisi zote za kanda kushiriki katika Iftar katika maeneo mbalimbali. Aliongeza kuwa hatua hiyo imewapa wanawake fursa ya kuungana, kushirikiana na kuimarisha mshikamano wao, na kuwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wa watumishi wanawake katika kufikia malengo ya taasisi.
Iftar hiyo iliwakutanisha wafanyakazi wanawake wa HESLB pamoja kwa lengo la kuimarisha mshikamano, kujenga mahusiano mazuri mahali pa kazi na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya taasisi na jamii kwa ujumla, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Tukio hilo lilihitimishwa kwa dua na futari ya pamoja, ikiwa ni ishara ya umoja, upendo na kuthamini mchango wa wanawake katika taasisi na jamii.
Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050”, kwa Mkoa wa Dar es Salaam yatafanyika kesho, Jumapili, Machi 8, 2026 katika Viwanja vya Mburahati Barafu.