Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, jana (Julai 26, 2026), alifunga rasmi Maonesho ya Sita ya Wiki ya Elimu Pemba yaliyofanyika katika Viwanja vya Gombani, Pemba, huku akisisitiza umuhimu wa maonesho hayo katika kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu fursa na huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za elimu.
Maonesho hayo yamezikutanisha taasisi mbalimbali za elimu na wadau wa sekta ya elimu kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi, pamoja na kusogeza karibu huduma mbalimbali zinazohusu elimu.
Katika maonesho hayo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB) ilishiriki kikamilifu kwa kutoa elimu kuhusu huduma za mikopo ya elimu ya juu, vigezo vya kupata mkopo, kutoa usaidizi wa moja kwa moja kwa waombaji wa mikopo, pamoja na taratibu za kurejesha mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB), Bi. Umrat Suleiman Mohammed, alitembelea banda la HESLB ambapo alipata fursa ya kujionea huduma zinazotolewa kwa wananchi na namna maafisa walivyokuwa wakitoa elimu kuhusu mchakato wa maombi ya mikopo ya elimu ya juu.
Aidha, vijana kutoka Umoja wa Watu wenye Ulemavu walifika katika banda la HESLB kwa ajili ya kupata elimu kuhusu fursa za mikopo ya elimu ya juu na kupatiwa usaidizi wa kujaza na kuwasilisha maombi yao ya mkopo. Hatua hiyo ilidhihirisha dhamira ya kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi na kuwawezesha makundi mbalimbali kupata taarifa na huduma zinazohitajika.
Ushiriki wa HESLB katika Maonesho ya Wiki ya Elimu Pemba umeendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuelimisha umma kuhusu fursa za ufadhili wa elimu ya juu, kuongeza uelewa kuhusu taratibu za utoaji na urejeshwaji wa mikopo, pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa elimu na wananchi, kutoa elimu, kujibu maswali na kuhamasisha vijana kutumia fursa zilizopo za kujiendeleza kielimu kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.