Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeandaa na kufuturu na wadau wake wa kimkakati kwa lengo la kufahamiana, kuifahamu taasisi hiyo vizuri na kuimarisha mshikamano.
Hafla hiyo ya futari imefanyika Jumatano, Machi 11, 2026 katika Hotel ya Madinat Al Bahr, Zanzibar ambapo Mgeni Rasmi, Waziri wa Kilimo Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mhe Suleiman Masoud Makame, amewashukuru na kuwatakia dua njema viongozi wakuu wa nchi kwa kuweza kusimamia nchi vema na kwa amani.
Mhe. Makame amewataja Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa viongozi wanaoongoza nchi kwa umakini mkubwa.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu na kumwomba aweze kuwapa viongozi wetu moyo wa upendo na Imani”, amesema Mhe. Makame.
Aidha, katika hafla hiyo, Waziri Makame ameipongeza HESLB kwa kazi kubwa inayoifanya kuhakikisha wanafunzi wahitaji wanapangiwa mikopo huku akirejea ongezeko la bajeti kutoka TZS 570 bilioni mwaka 2021/2022 hadi TZS 916.7 bilioni mwaka 2025/2026; ongezeko ambalo linakwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi wanaonufaika na mikopo hiyo.
Awali, akitoa maneno ya utangulizi na shukrani kwa wadau wote walioshiriki katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia alisema kuwa HESLB imekuwa na utaratibu wa kuandaa futari maeneo mbalimbali ya nchi na kushirikiana na wadau wake kwa lengo la kuimarisha mshikamano na ushirikiano.
“Tumekuwa na utaratibu kama huu miaka ya hivi karibu kwa lengo la kufahamiana, kuifahamu taasisi yetu na kuimarisha mshikamano … Tutakuwa na shughuli kama hii Dar es salaam siku ya Jumamosi”, amesema Dkt. Kiwia.
Wadau takriban 200 walihudhuria hafla hiyo ya futari wakiwemo mawaziri wa sekta mbalimbali, viongozi wa mashirika ya umma na binafsi, viongozi wa dini, wafanyakazi na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.