7
Jul 2026

Kamanda Muliro aipongeza HESLB kwa Ubunifu wa “Kiduchu” na Mageuzi ya Kidijitali

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro, ameipongeza HESLB kwa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuimarisha ukusanyaji wa marejesho ya mikopo na kubuni kampeni ya urejeshaji kidogokidogo maarufu Kiduchu, ambao amesema utasaidia kuongeza ushiriki wa wadaiwa kurejesha mikopo ya elimu ya juu.

SACP M.J Muliro ametoa pongezi hizo leo alipotembelea banda la HESLB katika siku ya kilele cha Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Akiwa katika banda hilo, SACP M.J Muliro amesema HESLB imeendelea kuonesha dhamira ya kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu zinawanufaisha Watanzania wengi zaidi kwa kusimamia ipasavyo urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika wenye kipato waliohitimu masomo yao na kuajiriwa au kujiajiri.

Amesema juhudi za kuwafuatilia wadaiwa na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo ni hatua muhimu inayowezesha fedha hizo kuendelea kuwanufaisha wanafunzi wengine wanaostahili kupata mikopo kwa ajili ya kuendelea na masomo ngazi ya elimu ya juu.

Aidha, Kamanda Muliro ameipongeza HESLB kwa kuanzisha kampeni ya Kiduchu, akieleza kuwa ni ubunifu unaotoa nafasi kwa wadaiwa wenye vipato vya chini kuanza kurejesha mikopo yao kulingana na uwezo wao, hatua itakayoongeza hamasa ya urejeshaji na kuimarisha uendelevu wa mfuko wa mikopo ya elimu ya juu.

“Huu ni ubunifu mzuri ambao unawapa fursa hata wale wenye kipato kidogo kuanza kutekeleza wajibu wao wa kurejesha mikopo. Hii itaongeza mwitikio wa wadaiwa na kuwafanya wengi zaidi washiriki katika kuchangia elimu ya vizazi vijavyo,” alisema SACP M.J Muliro

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro ameisifu HESLB kwa kuendelea kuboresha huduma zake mwaka hadi mwaka kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali, akibainisha kuwa hatua hizo zimeongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Banda la HESLB limeendelea kuvutia mamia ya wananchi wanaotembelea maonesho hayo, ambao hupata fursa ya kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali zinazotolewa papo hapo.

Published: July 7, 2026 at 8:07 PM