Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ameipongeza Serikali kwa mafanikio makubwa katika kupanua wigo wa mikopo ya elimu ya juu, akisema ongezeko la uwekezaji kutoka TZS 500 bilioni hadi kufikia zaidi ya TZS trilioni 1 limewezesha vijana wengi zaidi kupata fursa ya elimu ya juu.
Mhe. Mtaka ameyasema hayo alipotembelea banda la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi yaliyofanyika Zanzibar kuanzia Agosti 12 hadi 14, 2026, ambapo alipata maelezo kuhusu taarifa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi.
“Kikubwa ni mafanikio makubwa yaliyofanyika katika Wizara ya Elimu, hususan kwenye eneo la mikopo ya elimu ya juu; kutoka kwenye safari ya Shilingi bilioni 500 mpaka sasa tunaongelea uwekezaji wa Shilingi trilioni 1. Unaona kabisa kwamba Serikali imeendelea kugusa kundi kubwa la vijana katika masomo ya elimu ya juu,” amesema Mtaka.
Amesema uamuzi wa Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupanua wigo wa mikopo umeleta manufaa makubwa kwa jamii, hususan kwa wazazi ambao watoto wao walikuwa wakikabiliwa na changamoto za kupata mikopo ya kugharimia elimu ya kati.
Aidha, Mhe. Mtaka amepongeza mpango wa ruzuku ya Samia Scholarship, akisema umeendelea kuwahamasisha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo ya sayansi ili kupata fursa ya kuendelea na masomo kupitia ufadhili huo.
“Lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa maamuzi ya kutoa Samia Scholarship kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi. Leo watoto wa Kitanzania wanashindana kwenye mitihani ya Kidato cha Sita wakiamini kwamba kufanya vizuri kutampa nafasi ya kuweza kusoma Samia Scholarship,” amesema.
Akizungumzia ushiriki wa HESLB katika maonesho hayo, Meneja wa HESLB Ofisi ya Zanzibar, Bw. Philbert Temba, amesema wamejikita kuhakikisha wananchi wanapata kwa wakati huduma na taarifa sahihi, huku wakitumia fursa hiyo kusogeza huduma za Bodi karibu zaidi na jamii.
“Tumelenga kuhakikisha kila anayefika katika banda letu anaondoka akiwa na taarifa sahihi kuhusu huduma za HESLB, … hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha hakuna anayekosa taarifa muhimu kwa sababu ya kutokufikiwa,” amesema Temba na kuongeza kuwa kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi, HESLB imekuwa ikipata fursa ya kuelewa changamoto na maswali yanayowakabili walengwa wake na hivyo kutoa ufafanuzi unaowezesha kujenga uelewa sahihi kuhusu utoaji na urejeshaji mikopo.
Kupitia ushiriki huo, HESLB imeendelea kutoa elimu na huduma kwa makundi mbalimbali, yakiwemo wanafunzi wanaotarajia kuomba mikopo, wazazi na walezi, wanufaika wa sasa wa mikopo pamoja na wanufaika waliomaliza masomo na wanaorejesha mikopo yao.