Wanafunzi 314 wameshiriki katika warsha ya kwanza ya ‘Imbeju-SmartElite’ iliyofanyika tarehe 7 Machi, 2026 katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), jijini Dar es Salaam ikilenga kutoa elimu juu ya umuhimu wa ujuzi wa kidijitali, matumizi ya teknolojia ya akili unde (AI), na elimu ya kifedha kwa vijana wa vyuo vikuu.
Miongoni mwa waliowasilisha mada katika warsha hiyo, ni pamoja na Bi. Catherine Rutenge kutoka Benki ya CRDB, wajasiriamali wa kidijitali waliotoa mifano hai ya namna vijana wanavyoweza kutumia teknolojia kujenga ajira na biashara endelevu, na Bw. Saleko Mandara, Afisa Mikopo Mkuu wa HESLB aliyezungumzia umuhimu wa wanafunzi kutumia fedha za mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Bw. Mandara alisisitiza kuwa nidhamu ya matumizi ya fedha ni msingi wa mafanikio ya kitaaluma na maisha ya baadaye ikiwa ni pamoja na kujiandaa kurejesha mkopo wa elimu ya juu mara mwanafunzi anapohitimu masomo yake, ambapo pia alielezea taratibu za kurejesha mkopo kwa wanufaika walioajiriwa na waliojiajiri.
Kwa mujibu wa Bw. Mandara, ushiriki wa HESLB katika warsha hizi ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wanapata si tu msaada wa kifedha, bali pia maarifa ya kuzitumia kwa ufanisi pamoja na stadi muhimu zitakazowawezesha kuwa na ushindani kwenye soko la ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeendelea kushirikiana na wadau wake wa kimkakati kutekeleza dhamira yake ya kuelimisha wanafunzi kuhusu matumizi sahihi ya mikopo ikiwa ni pamoja na fedha wanazolipwa wanafunzi kwa ajili ya chakula na malazi, na za kununulia vitabu na viandikwa.