Watumishi wa HESLB Ofisi ya Dodoma, leo (Jumatano, Machi 18, 2026) wamefanya matendo ya huruma kwa kupeleka msaada wa vitu mbalimbali katika Gereza Kuu la Isanga lililopo jijini Dodoma.
Akizungumza kuhusu tendo hilo, Meneja wa HESLB Ofisi ya Dodoma, Bi. Octavia Seleman amesema wameamua kutoa msaada katika gereza la Isanga ikiwa ni sehemu ya kuwakumbuka watu walio katika changamoto na wanaohitaji faraja.
“Tuwakumbuke watu walio katika changamoto, kama vile wafungwa kwani wanahitaji upendo na faraja kutoka kwetu”, amesema Bi. Octavia.
Watumishi hao wa HESLB wamepokelewa na mwakilishi wa Kamishna wa Magereza, ACP Atu Juvenile Namwata ambaye ametoa shukrani kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Magereza.
ACP Namwata amewashukuru wafanyakazi wa Bodi ya Mikopo kwa moyo wao wa kujitoa kwa sadaka walizozitoa.
"Kwa sasa Jeshi la Magereza linajitegemea katika kujiendesha, pamoja na miradi mingine … pia tunashukuru sana kwa sadaka zenu maana zinaongezea katika mahitaji ambayo wanafunzi wetu (akimaanisha wafungwa) hapa wanahitaji”, amesema ACP Namwata na kuongeza, “Tunawakaribisha sana hata kuja tu kuongea nao ili kuwapa maneno ya faraja maana yanawajenga kisaikolojia".