MPYA: UFAFANUZI WA ZIADA KUHUSU UTOAJI MIKOPO 2018-19

1.    Je, ikiwa jina la mwanafunzi lipo kwenye ‘Batch 1’ iliyotangazwa kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (HESLB) lakini jina lake halijatumwa chuoni afanye nini?

Jibu: Mwanafunzi ambaye jina lake lilitangazwa kwenye ‘Batch 1’ lakini halimo katika orodha zilizopo vyuoni kwa sasa, anatakiwa kusubiri kukamilishwa kwa mapitio ya ziada.

 

Hili ni kundi la wanafunzi ambao maombi yao yamebainika kuwa na upungufu wa aina mbalimbali ambao kwa sasa unapitiwa na watalaam kwa ajili ya kurekebishwa. Baada ya kazi hiyo kukamilika, taarifa zao zitatumwa vyuoni.

 

2.    Je, orodha ya Awamu ya Tatu (Batch 3) itatolewa lini?

Jibu: Bodi ya Mikopo inaendelea na upangaji mikopo na kupeleka fedha vyuoni. Orodha ya Awamu ya Tatu itatolewa  kuanzia tarehe 3 Novemba, 2018 na itatangazwa kupitia kwenye tovuti ya www.heslb.go.tz.

 

3.    Nitajuaje kiasi cha mkopo nilichopangiwa?

Jibu: Orodha ya majina kwa waliopangiwa mikopo pamoja na mchanganuo wa kiasi alichopangiwa kila mwanafunzi, hutumwa vyuoni walikodahiliwa kwa kuthibitisha udahili wao.

 

4.    Mwanafunzi aliyesajiliwa katika chuo tofauti, na mkopo wake kupelekwa chuo alichodahiliwa na kuthibitisha awali, anapaswa kufanya nini ili apate fedha za mkopo zilizopelekwa kwenye chuo cha awali?

Jibu: Mwanafunzi huyu anapaswa kukamilisha usajili (registration) katika chuo kipya alichopo na kumtaarifu Afisa Mikopo (Loan Officer) wa chuo hicho kipya. Baada ya hatua hii, taarifa zake zitawasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na baadae HESLB ili taarifa za udahili na mkopo wake vihamishiwe chuo chake kipya.

 

5.    Je, dirisha la kukata rufaa litafunguliwa lini?

Jibu: Baada ya kukamilisha upangaji wa mikopo, Bodi ya Mikopo (HESLB) itatangaza tarehe rasmi ya kufungua dirisha la rufaa. Kwa sasa, kazi ya upangaji mikopo kwa awamu zinazofuata inaendelea. Maelezo ya kina kuhusu dirisha la rufaa yatatolewa kuanzia tarehe 12 Novemba 2018 kupitia tovuti ya www.heslb.go.tz.

Imetolewa na:

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

DAR ES SALAAM

ALHAMISI, NOVEMBA 1, 2018

 

Kwa maswali, tupigie 0736 66 55 33 au 0739 66 55 33 (Saa 2:30 asubuhi – 11:00 jioni)