2,397 WAPATA MIKOPO AWAMU YA PILI

Kiasi cha shilingi bilioni 98.12 mpaka sasa kimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 27,929 kati ya wanafunzi 40,485 wa mwaka wa kwanza waliotarajiwa kupatiwa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Abdul-Razaq Badru imesema kuwa idadi ya wanafunzi waliobaki wapatao 12,556 watapangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 42 katika awamu inayofuata ili kukamilisha idadi iliyokusudiwa.

Idadi ya wanafunzi 27,929 waliokwishapangiwa mikopo na ambao wamedahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vinavyotambulika; ni asilimia 69 ya wanafunzi 40,485 wanaotarajiwa kunufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019.

Orodha ya majina ya wanafunzi hao  27,929 (Awamu ya kwanza 25,532 na awamu ya pili 2,397) waliokwishapangiwa mikopo inapatikana kwenye tovuti hii  na itatumwa kwenye vyuo husika kwa ajili ya hatua zaidi za kukamilisha malipo ya mikopo hiyo.

Wakati huo huo, Bodi imeendelea kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo na ambao wamefaulu masomo yao ya mwaka wa masomo 2017/2018.

Bodi inatarajia kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi 124,000 kwa mwaka wa masomo 2018/2019 wakiwemo wa mwaka wa kwanza 40,485 na wanaoendelea na masomo wapatao 83,515.

 

Hitimisho

Bodi ya Mikopo inawasisitizia waombaji wa mikopo wenye sifa ambao hawajapangiwa mikopo, kuendelea kuwa na subira wakati ikikamilisha orodha inayofuata ya wanafunzi waliopata mikopo. Taarifa zitaendelea kutolewa mara kwa mara kupitia vyombo vya habari na tovuti hii ya Bodi.

Imetolewa na:

ABDUL-RAZAQ BADRU

MKURUGENZI MTENDAJI

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

JUMATATU, OKTOBA 29, 2018