MPYA: MASWALI NA MAJIBU UTOAJI MIKOPO 2018/2019

 1.   Swali: Je, nitajuaje kama nimepata mkopo?

Jibu : Tembelea tovuti ya www.heslb.go.tz ili kuona orodha ya waliopata mkopo. Tumia namba yako ya mtihani wa kidato cha nne uliyotumia wakati wa kuomba mkopo kutafuta (search) jina lako.

2.     Swali: Iwapo jina langu halimo kwenye orodha ya waliopangiwa mikopo tayari nifanyeje?

Jibu : HESLB imetoa orodha ya Awamu ya Kwanza ya waliopata mikopo tarehe 17 Oktoba, 2018. Mchakato wa kupanga mikopo unaendelea, hivyo unashauriwa kusubiri awamu inayofuata ambayo itatolewa kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2018

3.     Swali: Nifanye nini iwapo HESLB itakamilisha kupanga mikopo kwa awamu zote na mimi nikakosa na ni muhitaji?

Jibu: HESLB hutoa nafasi kwa waombaji wote waliokosa mikopo na ambao wanaamini ni wahitaji kukata rufaa ili Bodi ya Mikopo iweze kupitia upya maombi yao ya mikopo. Rufaa zao huwasilishwa HESLB kupitia Ofisa anayesimamia masuala ya mikopo katika chuo husika. Tangazo la kukaribisha maombi ya rufaa litafunguliwa mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2018.

4.     Swali: Je, kama sijaridhika na kiwango cha mkopo nilichopangiwa, nifanye nini?

Jibu: Waombaji wote ambao wamekosa au hawajaridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa watapata nafasi ya kukata rufaa na kwa kufuata maelekezo yatakayotolewa kwenye tangazo litakalotolewa. Waombaji watapaswa kuweka vielelezo vya ziada vinavyoonyesha uhitaji wao ambavyo awali havikuambatanishwa. Dirisha la rufaa litafunguliwa tarehe 1 hadi 15 Novemba 2018. Tembelea www.heslb.go.tz kuanzia mwezi Novemba, 2018 kwa maelezo.

5.     Swali: Je, iwapo nimepata mkopo kisha nikaamua kuahirisha masomo, nitaruhusiwa kuomba tena?

Jibu: Mwombaji aliyekosa mkopo mwaka huu, anaruhusiwa kuomba mkopo upya kwa mwaka mwingine wa masomo kwa kuzingatia mwongozo wa utoaji mikopo wa mwaka ujao ambao utatoa maelekezo ya kina. Aidha, mwombaji wa mkopo anapaswa kuhakikisha anatoa taarifa rasmi kwa chuo chake kwa wakati. Taarifa hizo zitawasilishwa HESLB na chuo kwa ajili ya kumbukumbu.

6.    Swali: Je, nitajuaje kiasi cha mkopo nilichopangiwa?

Jibu: Orodha ya majina yenye kiasi cha fedha alizopangiwa mwanafunzi hutumwa chuoni na HESLB. Aidha, kwa kila mnufaika wa mkopo ataweza kujua kiasi cha mkopo alichopangiwa kupitia akaunti yake ya maombi ya mkopo baada ya siku chache tangu orodha itangazwe.

7.     Swali: Je, ni lini fedha za mikopo zitapelekwa vyuoni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza?

Jibu: Kwa wanafunzi ambao wameshapangiwa mikopo, fedha zao zinatumwa vyuoni na HESLB kabla ya vyuo kufunguliwa kuanzia tarehe 29 Oktoba, 2018.

Swali: Iwapo naendelea na masomo na sikupata mkopo mwaka uliopita, na nimeomba mkopo upya mwaka huu, nitajuaje kama nimepata?

Jibu: Wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao walioomba mkopo kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2018/2019 na wana sifa watapata taarifa za mikopo yao kwa maafisa mikopo wa vyuo vyao mara watakapowasili vyuoni. Mikopo kwa wanafunzi wa kundi hili hupangwa baada ya HESLB kupokea matokeo ya mitihani yao kutoka kwa uongozi wa vyuo vyao.

9.    Swali: Je, nifanye nini iwapo ninataka kuhamia chuo kingine kama nimekwisha pangiwa mkopo?

Jibu: 

·         Wasilisha taarifa zako kwa chuo ulichopo ili waijulishe Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

·         TCU watawasilisha taarifa zako kwa Bodi ya Mikopo (HESLB)

·         Fanya usajili katika chuo unachohamia na mpatie taarifa zako afisa mikopo wa chuo ulichohamia ili aziwasilishe Bodi ya mikopo (HESLB).

10.  Swali: Ikiwa nimeshafika chuoni, na nina swali kuhusu mkopo ninapaswa nifanye nini?

Jibu: Kila chuo kina afisa anayesimamia masuala ya mikopo ambaye anafanya kazi chini Mkuu wa Taaluma wa chuo husika. Ulizia ofisi yake na atakuhudumia.

 

Imetolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

 DAR ES SALAAM

OKTOBA 19 2018