MWISHO WA KUJISAJILI MAOMBI YA MKOPO

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu waombaji wa mikopo mwaka wa masomo 2018/2019 kuwa mfumo wa kupokea maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao https://olas.heslb.go.tz   utafungwa usiku wa leo, Jumanne, Julai 31, 2018.

Hata hivyo, waombaji ambao tayari wamejisajili katika mfumo na wapo katika hatua mbalimbali za maombi, wataruhusiwa kukamilisha maombi yao na kutuma nakala ngumu (hardcopies) za maombi ya mkopo kwa ‘EMS’ kupitia Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Tarehe ya mwisho ya kutuma fomu kwa ‘EMS’ ni Jumatano, Agosti 15, 2018 ili kutoa nafasi kwa HESLB kuchambua, kuhakiki, kupanga na kutoa orodha ya waombaji wenye sifa watakaopata mikopo kabla ya vyuo kufunguliwa.

Hadi kufikia leo, waombaji mikopo zaidi ya 76,000 wamewasilisha maombi yenye viambatisho vinavyotakiwa kwa njia ya mtandao. Maombi yote yatachambuliwa kwa kuzingatia sifa na vigezo vilivyotangazwa.

Uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo
Kuhusu kuwasilisha nakala za vyeti vya kuzaliwa vya waombaji wa mikopo na vile vya vifo vya wazazi waliofariki dunia, HESLB inafanya kazi kwa karibu na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao wanakamilisha uhakiki wa vyeti vyote walivyopokea.

HESLB itapokea orodha kamili yenye majina ya waombaji wote wa mikopo waliowasilisha vyeti RITA kwa ajili ya uhakiki ili kuoanisha na taarifa zilizowasilishwa na waombaji kwa njia ya mtandao na nakala ngumu.

Hivyo basi, waombaji wote wa mikopo ambao hadi sasa hawajapokea taarifa za uhakiki kutoka RITA, wapandishe (upload) nakala laini walizonazo katika mfumo wa maombi https://olas.heslb.go.tz na kutuma nakala ngumu kwa njia ya ‘EMS’ kama ilivyoelekezwa.

Hitimisho
Pamoja na ufafanuzi huu, tunapenda kuwakumbusha waombaji wa mikopo wanaokamilisha maombi yao kuzingatia maelekezo yaliyomo katika ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2018/2019’. Mwongozo huu unapatikana katika tovuti hii www.heslb.go.tz . Iwapo wana maswali, wawasiliane nasi kupitia:

Simu:         0736665533 au 022 5507910
Barua pepe:     This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.  au This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. 

Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Jumanne, Julai 31, 2018