BODI YA WAKURUGENZI YAWAACHISHA KAZI WATUMISHI SITA

Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeamua kuwaachisha kazi watumishi sita (06) wa Bodi ambao walisimamishwa kazi mwaka 2016 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yao. Uamuzi huu umefanyika katika kikao cha Bodi kilichofanyika Jumanne, Juni 12, 2018 jijini Dar es Salaam.
Watumishi walioachishwa kazi ni:
i.  Bw. Juma Hamisi Chagonja – Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo;
ii.  Bw. Onesmus Ngitiri Laizer – Mkurugenzi wa Upangaji na Ugawaji Mikopo;
iii.  Bw. John N. Elias – Mkurugenzi Msaidizi wa Ugawaji Mikopo;
iv.  Bw. Robert L. Kibona - Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo;
v.  Bw. Heri L. Sago – Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu; na
vi.  Bw. Chikira L. Jahari – Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo.

Watumishi hao wamekutwa na makosa ya uzembe uliokithiri, kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma 2002 na Kanuni zake, Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178), Kanuni za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu zinazoongoza majukumu yao; na kusababisha hasara ya upotevu wa fedha za Serikali kiasi cha shilingi 7.1 bilioni.

Uamuzi wa Bodi umechukuliwa baada ya kupokea na kujadili taarifa ya Kamati ya Uchunguzi (Inquiry Committee) iliyojumuisha wataalam wa sheria, fedha na utumishi wa umma kwa lengo la kufanya uchunguzi na mahojiano na watuhumiwa hao.
Kufuatia uamuzi huu, wahusika wote wamepewa taarifa ikijumuisha haki yao ya kukata rufaa kwa Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 45 endapo hawajaridhika na uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi.

Bodi ya Wakurugenzi pia imewakumbusha watumishi wote wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo halali inayotolewa. Watumishi wa Bodi pia wametakiwa kuzingatia uadilifu na umakini ili kuepuka vitendo vinavyoweza kuisababishia hasara Serikali.


Imetolewa na:

Abdul-Razaq Badru
Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Jumatano, Juni 13, 2018