WIKI YA UTUMISHI WA UMMA TAREHE 19 HADI 23 JUNI

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawakaribisha wadau wake wote kuja kupata huduma mbalimbali katika maeneo ya Utoaji mikopo na Urejeshaji mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kuanzia tarehe 19 hadi 23 Juni, 2017.

Katika kipindi hiki chote; dawati la huduma kwa wateja litakuwepo kwenye lango kuu la kuingilia Ofisi za Bodi zilizopo Mwenge, Dar es Salaam kuanzia saa 2.30 asubuhi hadi saa 11.00 jioni. Wadau watajibiwa maswali na kupewa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya Utoaji Mikopo hususan kwa Mwaka wa masomo 2016/2017 na maandalizi ya mwaka wa masomo 2017/2018.

UTUMISHI

Kuhusu Urejeshaji wa Mikopo; Taarifa za kiasi cha mkopo anaodaiwa mnufaika zitatolewa papo hapo na Wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao wataweza kujaza fomu za maulizo (inquiry forms) kwa kutoa taarifa zao za sasa ili Bodi iweze kuanza kukusanya mikopo kutoka kwao.

Kwa upande wa Utoaji mikopo; wadau watapata fursa ya kujua vigezo vinavyotumiwa, utaratibu wa kuomba hadi kupangiwa mikopo, viwango vya mikopo vinavyopangwa; utaratibu wa kukata rufaa na iwapo kuna tatizo la utoaji mikopo kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taarifa za mwombaji mkopo.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu pia imeandaa machapisho yenye taarifa za utoaji na urejeshwaji mikopo ili kuwagawia wadau watakaotembelea ofisi yake.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ina watumishi wenye uzoefu na weledi katika masuala ya utoaji na urejeshwaji wa mikopo na hivyo wadau watarajie kupatiwa huduma bora.

Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU