Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


24
June 2024

HESLB YASHEREHEKEA 'MIKOPO OPEN DAY' 2024

  • YATUNUKU WAAJIRI ZANZIBAR

Zanzibar, Juni 20, 2024

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia ametoa tuzo za mwaka 2023/2024 kwa Taasisi kumi zilizopo Zanzibar kwa kutambua mchango wao katika urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi na kufuata Sheria ya HESLB ipasavyo.

Akiongea katika hafla fupi ya utoaji tuzo ambayo pia ilitumika kusherehekea ‘Mikopo Open Day’ inayoadhimishwa kila mwaka kukumbuka kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwezi Juni, 2004, Dkt. Kiwia alizipongeza taasisi zilizotunukiwa kwa kuonesha ushirikiano na umakini katika kutambua dhima ya HESLB ya kuhakikisha fedha zilizopeshwa kwa wanafunzi zinarejeshwa ili kuwezesha wanafunzi wengine wa kitanzania kutimiza ndoto zao za kufikia elimu ya juu.

“Tuendelee kushirikiana katika kuwasisitiza waajiriwa waliopo katika maeneo yetu ambao ni wanufaika ili waweze kurejesha mikopo yao kwa wakati …sote tuwe mabalozi kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kurejesha mikopo”, alisema Dkt Kiwia.

Naye Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshawaji Mikopo, CPAT George Mziray aliwaeleza waajiri kuwa HESLB imeendelea kuboresha mifumo yake ya urejeshaji mikopo ili kuwawezesha waajiri na wanufaika kukamilisha taratibu zote kupitia kwenye mifumo bila kulazimika kufika ofisi za HESLB.

“Tuna mifumo ya wanufaika mmoja-mmoja (LIPA), ya waajiri wanaofuata sheria (EPO) na pia kwa ajili ya waajiri ambao hawafuati sheria (COPO) ili kuwawezesha kulipa kiasi walichoelekezwa”, alisema Mziray.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) uliopo katika Jengo la Michenzani Mall, Zanzibar, Taasisi zilizotunukiwa ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais: Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar. Taasisi nyingine ni ASA Microfinance Zanzibar Limited, DNATA Zanzibar Aviation Service Company Limited, Glorius Academy na Zanlink.

Awali, Meneja wa HESLB, Ofisi ya Zanzibar, Philbert Temba alisema kuwa taasisi nyingi za Zanzibar zinafanya vizuri katika marejesho lakini taasisi kumi zilizotunukiwa zimejipambanua zaidi kwa kuwasilisha majina ya wanufaika walioajiriwa, kukata 15% ya mishahara yao na kuwasilisha HESLB ndani ya siku 15 kama sheria ya HESLB inavyoelekeza.

Temba alisema kuwa taasisi hizo zimeenda mbele zaidi ya kutekeleza sheria, “siyo kwa kutimiza tu matakwa ya kisheria, lakini pia taasisi hizi zimekuwa na ushirikiano na mawasiliano ya karibu na HESLB kuhusu waajiriwa walionufaika na mikopo na kuhakikisha makato hayo yanafanyika mapema”.

Hii ni mara ya pili kwa waajiri wa Zanzibar kutunukiwa ngao na HESLB kwa kutambua ushirikiano wao katika kurejesha mikopo ya elimu ya juu. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi Aprili mwaka 2018 ambapo tuzo zilitolewa kwa taasisi tano zilizokuwa zimefanya vizuri kwa mwaka 2017/2018. Taasisi hizo zilikuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Fedha na Mipango, Shule za Feza Zanzibar, Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).