Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


13
March 2023

Wadau kutafakari ugharimiaji elimu ya juu jijini Dodoma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeandaa Kongamano la kwanza la tafakuri ya ugharimiaji wa elimu ya juu litakalofanyika Alhamisi, Machi 16, 2023 katika Hoteli ya Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, ufunguzi wa kongamano hilo utafanywa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) na kufungwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo.

“Baada ya miaka takribani 18 ya utoaji mikopo ya elimu ya juu tangu HESLB ianzishwe mwaka 2005, tunaamini ni muda muafaka wa kufanya tafakuri ili kuwa na uelewa wa pamoja wa fursa na changamoto zilizopo,” amesema Badru.

Katika kongamano hilo, mada kuu tatu zinatarajiwa kuwasilishwa na wataalamu ambazo zinatokana na tathmini walizofanya. Mada hizo ni ‘Ukusanyaji wa Rasilimali kwa Ugharimiaji wa Elimu ya Juu Tanzania’ itakayowasilishwa na Dkt. Mariam Tambwe, mhadhiri kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dar es salaam.  

Mada nyingine ni ‘Athari za Kijamii na Kiuchumi Zinazotakana na Ugharimiaji wa Elimu ya Juu’ itakayowasilishwa na Dkt. Martin Chegere kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM); na ‘Usimamizi na Vipaumbele katika Ugharimiaji wa Elimu ya Juu’ itakayowasilishwa na Dkt. Muhajir Kachwamba, Kamishna Msaidizi, Wizara ya Fedha na Mipango.

Washiriki wa kongamano hilo ni wadau wa elimu ya juu zikiwemo taasisi za elimu ya juu, wanafunzi, sekta binafsi, taasisi za fedha na waajiri.

Kupitia kongamano hili, maoni mbalimbali yatapokelewa na hivyo kusaidia katika kuboresha na kuongeza ufanisi wa utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu nchini.