Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


15
September 2021

HESLB, TASAF KUWEZESHA WANAOTOKA KAYA MASKINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo ameitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuhakikisha watanzania wahitaji wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu wanawezeshwa.

Akizungumza katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Sebastian Inoshi, wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya HESLB na TASAF iliyofanyika leo Jijini Dodoma, Dkt. Akwilapo amesema upo umuhimu kwa taasisi za Serikali kushirikiana katika kuwafikia wananchi na kutoa huduma.

Dkt. Akwilapo aliongeza kuwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha Watanzania wahitaji wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu wanapata mikopo na kutimiza ndoto zao, na kwamba upo umuhimu kwa HESLB na TASAF kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kama inavyotarajiwa.

“Katika hili naomba niwape takwimu, mwaka 2019/2020, Serikali ilitoa TZS 450 Bilioni zilizowanufaisha wanafunzi 132,392. Bajeti hii imeongezeka hadi kufikia TZS 570 Bilioni mwaka huu wa fedha 2021/2022 ambazo zitawanufaisha wanafunzi 160,000”, alisema Dkt. Akwilapo.

Aidha Dkt. Akwilapo alizitaka HESLB na TASAF ziongeze kasi ya kuunganishwa kwa mifumo yao ya TEHAMA ili kuwezesha utambuzi wa haraka na uhakika wa wanafunzi wanaotoka katika kaya masikini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaopata udahili katika taasisi za elimu ya juu nchini na ambao wapo katika mpango wa TASAF wanapata mikopo ili kutimiza ndoto zao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga amesema taasisi hiyo itahakikisha inasimamia kwa umakini malengo ya ushirikiano huo ili kuhakikisha wanafunzi wahitaji wanaotoka katika kaya maskini wanapata mikopo ya elimu ya juu kutoka HESLB.