The United Republic of Tanzania
HIGHER EDUCATION STUDENTS' LOANS BOARD

Wanafunzi wapya 3,544 wapangiwa mikopo ya TZS 11.04 bilioni


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya Awamu ya Tatu yenye jumla ya wanafunzi wapya 3,544 waliopangiwa mikopo kwa mara ya kwanza katika mwaka wa masomo 2020/2021 yenye thamani ya TZS 11.04 bilioni.

Ili kupata taarifa za kina kuhusu mikopo waliyopangiwa, wanafunzi hao 3,544 wanashauriwa kutembelea akaunti zao walizotumia kuomba mikopo kwa njia ya mtandao maarufu kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account (SIPA).

Kufuatia kutolewa kwa awamu hii ya tatu, hadi sasa jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ni 53,364 yenye thamani ya TZS 173.29 bilioni. Aidha, jumla ya wanafunzi 69,625 wanaoendelea na masomo wamepangiwa TZS 247.5 bilioni baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka 2019/2020.

Kufunguliwa kwa dirisha la rufaa

Baada ya kutangwa kwa Awamu ya Tatu, hatua inayofuata ni kufunguliwa kwa dirisha la rufaa kwa siku saba (07) kuanzia kesho (Jumatano, Desemba 2, 2020) ili kuwawezesha waombaji ambao hawajapangiwa mikopo au hawajaridhika na viwango walivyopangiwa kuambatisha nyaraka za ziada kuthibitisha uhitaji wao.

Katika kipindi cha rufaa, wanafunzi watahitajika kutembelea mfumo wa olas.heslb.go.tz, kufuata maelekezo na kuwasilisha rufaa zao kutoka popote walipo BILA MALIPO YOYOTE kwa HESLB.

Wito

HESLB inatoa wito kwa wanafunzi ambao bado hawajapangiwa mikopo na ni wahitaji, kutumia muda wa siku saba (07) za rufaa kuwasilisha nyaraka sahihi ili hatimaye wapangiwe mikopo ya kuwawezesha kulipia gharama za masomo.

Imetolewa na:

Abdul-Razaq Badru

Mkurugenzi Mtendaji,

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,

Dar es Salaam,

Desemba 1, 2020