| Bodi mpya ya Wakurugenzi yazinduliwa |
|
Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Dk. Shukuru Kawambwa.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za HESLB, Msasani, Dar es Salaam, Mh. Dk. Kawambwa aliwaeleza wajumbe wapya kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha kuwa HESLB inaendelea kutoa huduma bora na ufanisi wa hali ya juu kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaohitaji mikopo. Uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo unazingatia uwakilishi wa wadau mbalimbali wa elimu ya juu ambao ni pamoja na Wizara za Elimu, Wizara ya Fedha, Benki Kuu, Waajiri, Taasisi za Elimu ya Juu za umma na binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ina wajumbe 15 wakiwemo Mwenyekiti na Katibu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB.
Tangu kuanza kwa HESLB mwaka 2005, pamekuwa na bodi mbili za wakurugenzi kwa vipindi vya miaka mitatu mitatu. |
Uteuzi wa wajumbe wa bodi mpya ya wakurugenzi ulianza rasmi Aprili mosi 2011 na wajumbe hao wataisimamia HESLB katika mapendekezo na maamuzi ya kisera kwa muda wa miaka mitatu hadi Machi 31, 2014.