Dkt. Akwilapo azindua Baraza la Wafanyakazi HESLB

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amefungua mkutano wa siku moja wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) uliofanyika mjini Bagamoyo na kuwataka watumishi kuzingatia uadilifu na kuimarisha ushirikiano katika utendaji kazi wao.


“Baraza la Wafanyakazi mahali pa kazi lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kunakuwepo maelewano, ushirikiano na mshikamano kati ya wafanyakazi na uongozi,” amesema Dkt. Akwilapo katika mkutano huo uliofanyika  Juni 1, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.

BARAZAAmeongeza kuwa Baraza lihakikishe kunawepo na nidhamu ya kazi kwa madhumuni ya kuleta tija na ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za HESLB ili kuhakikisha malengo ya Serikali kuanzisha HESLB yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Pamoja na wito huo, Dkt. Akwilapo pia amewapongeza watumishi wa HESLB kwa kutekeleza majukumu yao ya kutoa na kukusanya mikopo ya elimu ya juu kwa ufanisi.


“Mmekuwa mkifanya kazi kwa bidii na kutoa taarifa kwa umma na hivyo kupunguza malalamiko kwa kuwa wananchi wanaelewa mnachokifanya,” amesema Katibu Mkuu.


Awali akimkaribisha Dkt. Akwilapo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali kupitia HESLB imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaokopeshwa kutoka wanafunzi 28,383 mwaka 2016/2017 hadi wanafunzi 33,941 mwaka huu wa masmo 2017/2018.

Aidha, Bw. Badru amesema kuwa kasi ya kukusanya fedha za mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika nayo imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Mwaka 2015/2016 tulikusanya TShs 28bn na makusanyo hayo yameongezeka hadi kufikia Tshs 130bn katika miezi tisa tu ya mwaka wa fedha 2017/2018, yaani Julai 2017 hadi Machi, mwaka huu,” amesema Bw. Badru.

Kuhusu malengo kwa mwaka 2018/2019, Bw. Badru amesema Serikali imetenga Tshs 427bn kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 40,000 na wanaoendelea na masomo zaidi ya 80,000.

Aidha, HESLB inakamilisha taratibu za kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada (Diploma) mbalimbali katika utaratibu ambao utatangazwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2018.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Dkt. Dalmas Nyaoro, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Menejimenti na wawakilishi wa Idara na Vitengo vya HESLB.