Bodi mpya ya Wakurugenzi yazinduliwa

Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezinduliwa leo Oktoba 3, 2017 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na kuitaka bodi hiyo mpya kufanyia kazi changamoto za kiutendaji na usimamizi ili kuweza kukidhi matarajio ya Watanzania.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za HESLB, Mwenge, Dar es Salaam, Mhe. Prof. Ndalichako aliwaeleza wajumbe wapya wa bodi kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa HESLB inaendelea kutoa huduma bora na ufanisi wa hali ya juu kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaohitaji mikopo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.

UZINDUZIWaziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akimkabidhi vitendea kazi Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya  Wakurugenzi Bi. Madina M. Mwinyi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya  Wakurugenzi Bi. Madina M. Mwinyi akimwalikilisha Mwenyekiti, katika salamu za shukrani, amemuahidi Waziri kuwa yeye na wajumbe wote wa bodi hiyo mpya watatumia uzoefu na utaalam wao katika Sekta ya elimu ya juu ili kuboresha mahusiano na wateja wa HESLB na pia kuweka vizuri kumbukumbu za utoaji na urejeshwaji wa mikopo.

Uteuzi wa wajumbe wa bodi mpya ya wakurugenzi ulianza rasmi Agosti mosi 2017 na wajumbe hao wataisimamia HESLB kuboresha utoaji huduma kwa muda wa miaka mitatu hadi Julai 31, 2020.

Uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo unazingatia uwakilishi wa wadau mbalimbali wa elimu ya juu kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ikiwa na wajumbe 9.

Bodi mpya inajumuisha Mwenyekiti Prof. William A.L. Anangisye na wajumbe ni Bi. Madina M. Mwinyi,  Bw. Gerson Mdemu, Mhandishi Dk. Richard Masika, Prof. Caroline Nombo, Dk. Dalmas A.L. Nyaoro, Bw. Frank Nyabudege Mugeta, Bi. Suzanne Urio, na nafasi ya mjumbe mmoja kutoka Wizara ya Fedha Zanzibar ambayo itajazwa baadaye.