HESLB YAMTUZA MFANYAKAZI HODARI 2016/2017

Katika kutambua mchango wake wa bidii na kujituma bila kuchoka, Bi. Zahra Kitara ameibuka kuwa Mfanyakazi hodari miongoni mwa wafanyakazi wote wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kipindi cha mwaka 2016/2017.
Zahra ambaye ni Afisa Mikopo daraja la kwanza katika Kitengo cha Uchambuzi na Upangaji Mikopo, alihitimu Shahada yake ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) mwaka 2010 na kujiunga na HESLB mwaka 2012. Kwa sasa yuko katika hatua za mwisho za kukamilisha Shahada ya Umahiri katika Uchumi katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Zahra Kitara

      Bi. Zahra Kitara

 Mshindi huyo wa jumla amesema siri yake kubwa imekuwa ni kujihoji kuhusu utendaji wake wa kazi wa siku hadi siku akihakikisha anaondoa makosa na kuboresha kazi zake, “mimi nimejiruhusu kuwa mtu wa kwanza kujipa changamoto mwenyewe, najua kuna maeneo fulani labda jana sikufanya vizuri, nafikiria leo nifanyeje ili niweze kuboresha na kufurahia kazi zangu”, alibainisha Zahra.
Awali akikabidhi vyeti na zawadi kwa Watumishi walioibuka bora kutoka Idara na Vitengo mbalimbali kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za makao makuu ya HESLB, Dar es Salaam, Jumatano Mei 10, 2017, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Abdul-Razaq Badru aliwapongeza walioibuka washindi lakini pia aliwapongeza wafanyakazi wote akisema juhudi za pamoja ndizo zimewawezesha walioibuka na kutunukiwa kufikia hatua hiyo.
Wengine walioshinda kutoka idara na vitengo mbalimbali ni Joyce Mgaya (Habari na Mawasiliano), Luhano Lupogo (Sheria), Saumu Mbwana (Utawala), Anthony Ooko (Uhasibu), Hidaya Karunde (Ukaguzi wa Ndani), Simon Manangu (TEHAMA), Sophia Saidan (Urejeshaji Mikopo), na Henry Kapinga (Manunuzi).
Menejimenti ya Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti (RAAWU) tawi la HESLB, kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kuwapongeza watumishi wanaojipambanua katika utendaji wao wa kazi ili kuongeza hamsa na tija miongoni mwao.

MWISHO