Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


18
May 2020

Prof. Ndalichako aitaka HESLB kujiandaa vyuo vikifunguliwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameielekeza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kujiandaa kulipa wanafunzi wakati wowote vyuo vitakapofunguliwa. Waziri ametoa maelekezo hayo leo (Jumatatu, Mei 18, 2020) katika ziara yake ya kikazi jijini Dar es salaam ambapo amekutana na menejimenti ya HESLB. ”Katika kipindi hiki ambapo vyuo vya elimu ya juu vimefungwa, HESLB ihakikishe inatumia muda huu kufanyia kazi changamoto zote za wanafunzi ili vyuo vitakapofunguliwa malipo ya mikopo wanafunzi yafanyike kwa wakati,” amesema Waziri katika ofisi za HESLB zilizopo karibu na makao makuu ya TAZARA. Katika ziara hiyo, Waziri pia aliipongeza HESLB kwa kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais kuhusu taasisi za umma kuhamia kwenye majengo ya Serikali. “Ninaamini hapa mtafanya kazi kwa utulivu na kutaongeza ufanisi katika kazi,” amesema Waziri. Prof. Ndalichako pia alitumia ziara hiyo kuwakumbusha watumishi wa HESLB kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona. Katika ziara hiyo Prof. Ndalichako alikagua ofisi ya urejeshaji mikopo na TEHAMA na kujionea watumishi wa HESLB wakiendelea kutekeleza majukumu yao. Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (kushoto) akipata ufafanuzi toka kwa Mkuregenzi mtendani wa HESLB, Bw. Abdul-Razaq Badru Akiongea katika kikao kati ya Waziri na menejimenti ya HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema HESLB ipo tayari kuwahudumia wanafunzi muda wowote vyuo vitakapofunguliwa. “Sisi tupo tayari. Serikali ilishatupa fedha na tutawawezesha wateja wetu mara moja vyuo vikifunguliwa”, amesema Badru. Badru ameongeza kuwa taasisi yake inakamilisha mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa kushirikisha wadau wakiwemo wanafunzi kupitia shirikisho lao, TAHLISO. Kuhusu urejeshaji wa mikopo iliyoiva, Badru amesema TZS 160 bilioni zimekusanywa katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, Julai 2019 hadi Aprili 2020. HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.